Hali katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamache imekuwa mbaya zaidi Kufuatia mvua mkubwa inayonyesha katika eneo la Kisii.
Hii ni baada ya maji ya mvua kujaa katika Hospitali hiyo, hali ambayo imehatarisha zaidi afya ya wagonjwa waliolazwa kwenya wodi za Hospitali hiyo.
Uchunguzi katika Hospitali hiyo umeonyesha kuwa kutokana na Hospitali hiyo kujengwa katika eneo la maji na kupelekea vyoo kufurika mvua inaponyesha na kusomba uchafu wote kutoka kwenye vyoo hivyo hadi kwenye wodi za wagonjwa.
Hali hii inakuwa mbaya zaidi kwa sababu mtaro unaoelekeza maji kutoka barabara ya Nyamache kuelekea Nyweera haupishi maji.
Hii imepelekea wagonjwa kwenye Hospitali hiyo kulalamika na kusema kwamba wanatatizika hata kutumia vyoo haswa wakati wa mvua.
Wagonjwa hao sasa wameomba Serikali ya Kaunti ya Kisii kuingilia kati na kuhahakisha shida hiyo imesuluhishwa haraka iwezekanavyo, ili kuepuka magonjwa yanayoletwa na uchafu kama hizo.
Kulingana na mhudumu mmoja wa afya katika Hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, usimamizi wa Hospitali ya Nyamache umeandikia Wizara ya Afya ya Kaunti ya Kisii kuhusu shida hiyo, lakini bado hamna hatua yoyote ambayo imechukuliwa.
Waziri wa Afya katika Kaunti ya Kisii Sarah Omache amesema kwamba ofisi yake tayari imefanya mazungumzo na Wizara ya Ujenzi ili kurekebisha hali hiyo.