Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed amepiga marufuku kesha za harusi kwa sababu za kiusalama.

Share news tips with us here at Hivisasa

Maalim amesema hatua hiyo inatokana na kukithiri kwa visa vya uhalifu vinavyotekelezwa wakati wa kesha za harusi katika sehemu mbali mbali Mombasa.

Akizungumza siku ya Jummane alipokutana na makundi ya wanawake eneo la Tudor, Maalim alisema harusi zote za usiku zinapaswa kukamilika ifikapo saa nne za usiku.

Kamishna huyo alisema kuwa yeyote atakayetaka kuendelea zaidi ya hapo basi atalazimika kugharamika kwa kukodisha walinda usalama kutoka kwa serikali.

“Ningetaka kwa heshima kuu, harusi zote zifikie kikomo saa nne za usiku. Iwapo unataka kuendelea zaidi ya hapo, utalazimika kugharimika kwa kukodisha walinda usalama kutoka kwa serikali ili kuweka ulinzi,” alisema Maalim.

Aidha, Maalim alisema kuwa kijana atakayepatikana na silaha aina yoyote atakabiliwa kama mhalifu bila ya kuzingatia umri wake.

Alisema kuwa hatua hiyo ni moja wapo ya mikakati ya kuboresha usalama katika kaunti ya Mombasa, inayokumbwa na changamoto ya magenge ya uhalifu haswa vijana wenye umri mdogo wanaohangaisha wananchi.