Kesi ya ufisadi inayomkabili Mwakilishi wa Wadi ya Shanzu Maimuna Salim imeahirishwa katika Mahakama ya Mombasa.
Hii ni baada ya Hakimu mkuu Susan Shitub kusema hayuko tayari kusikiliza kesi hiyo kwa sababu zisizo epukika siku ya Jumatatu.
Hatua hii ilimghadhabisha wakili Odour Siminyu na kuitaka mahakama kuharakisha kusikiliza kesi hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Odour alisisitiza kuharakishwa kwa kesi hiyo ili mteja wake apate fursa ya kugombea kiti cha uwakilishi Wadi ya Shanzu mwaka ujao.
Maimuna anadaiwa kuiitisha hongo ya shilingi laki tano kutoka kwa Maureen Aketch mnamo Julai 16, 2015 ili amsaidie katika kutatua mzozo wa ardhi baina yake na serikali ya kaunti.
Aidha, mwanasiasa huyo alikabiliwa na mashtaka mengine ya kuwatishia maafisa kutoka kitengo cha kupambana na ufisadi walioongozwa na Alfred Mwachugha, sawia na madai ya kuchochea wananchi kuchome gari la maafisa hao waliokuwa wakifanya uchunguzi dhidi yake.
Maimuna alishtakiwa pamoja na Christopher Karisa, aliyedaiwa kupokea hongo ya shilingi laki tano kwa niaba yake.
Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 26, 2016.