Share news tips with us here at Hivisasa

Mke wa raia wa kigeni ambaye ni miliki wa magari mawili yanayodaiwa kuibwa na mwakilishi wadi ya Kongowea Jabez Mdhai, amekiri kuwa mwakilishi huyo hakuiba magari hayo.

Akizungumza siku ya Jumapili kwenye kikao na wanahabari jijini Mombasa, Lilian Odhiambo, ambaye ni mke wa raia huyo wa kigeni, Joackim Steward amesema kuwa walielewana na Mdhai kuhusu umiliki wa magari hayo alipokuwa amekumbwa na matatizo ya kifedha baada ya kuteswa na mumewe.

Lilian amekiri kupokea shilingi milioni 1.8 kutoka kwa mwakilishi wadi huyo ili kujikimu kimaisha.

Aidha, aliongeza kuwa mumewe alimkana pamoja na watoto wake wadogo wawili, hali iliyomfanya kuteseka kimaisha.

Wakati huo huo, Mdhai alikana madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Liliana kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa, huku akisisitiza kuwa jambo hilo limeingizwa siasa ili kumchafulia jina uongozi wake.

Kiongozi huyo alitiwa mbaroni siku ya Ijumaa kwa madai ya kughushi stakabadhi ili kumiliki magari hayo aina ya Harrier na Mercedes Benz, ambazo ni mali ya raia wa kigeni, Joackim Steward.