Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama moja ya Nakuru siku yaJumanne ilifahamishwa kwamba kijana aliyeshtakiwa kwa kueneza ujumbe wa kuogofya kuhusiana na ugaidi kwenye ukurasa wa Facebook katika chuo kikuu cha Egerton aliandika ujumbe huo kupitia simu yake ya mkono.

Robert Mungai, anayefahamika kwa jina lingine Mohammed Bluez, anashtakiwa kutekeleza hatia hiyo wakati ambapo bewa la chuo kikuu cha Moi mjini Garissa lilivamiwa na kusababisha maafa ya watu 142 wengi wao wakiwa wanafunzi.

Afisa mtafiti wa uhalifu alikuwa amefahamisha mahakama kwamba alitumia teknolojia ya kiforensiki kama inavyohitajika na mahakama ili kupekua historia ya mshukiwa, ambapo aligundua kwamba Mungai alikuwa ametumia simu yake aina ya Samsung kuingia kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mtaalamu Antony Njue, alisema kwamba picha aliyokuwa ameweka Mungai kwenye akaunti yake ilikuwa na sura za washukiwa sugu wa ugaidi, ikiwemo ya Osama Bin Laden na ‘White lady’. Hata hivyo alisema hakupata ushahidi mwingine wa kumshuku.

Shahidi aliyetoa ushahidi wake alitafsiri jumbe ambazo zilikuwa za kiarabu zikidaiwa kuandikwa na Mungai.

Afisa wa polisi Mohammed Hassan aliiambia mahakama kwamba maneno ya kiarabu “arakat al shabaab al muhijadin” yalimaanisha vuguvugu la vijana lenye lengo la kujifahamisha na dini ya kiislamu.

Hata hivyo, alisema kwamba hakujua kama mshukiwa anaelewa kuzungumza kiarabu au la.

Mungai amekuwa kizuizini tangia kukamatwa kwake baada ya familia yake kushindwa kupata bondi ya shilingi 750, 000, na alikanusha mashtaka yote mbele yake.

Ujumbe anaodaiwa kuandika ulisoma 'hatufanyi mzaha, na kama unadhani tunafanya mzaha, tusubiri twaja. Garisaa sio kitu ikilinganishwa na yatakayofanyika chuo kikuu cha Egerton….Tunawapelelezi na ramani za Egerton yote'.

Mtaalamu mwingine kutoka kampuni moja ya mawasiliano anatarajiwa kuhojiwa mnamo Februari 2, 2016.