Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Photo/ the-star.co.ke]
Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Aisha Hussein Mohammed amepata afueni baada ya mahakama kuu ya Mombasa kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wake wa uchaguzi wa Agosti nane.Kesi ya kupinga ushindi wa Mohammed iliwasilishwa mahakamani na mpiga kura Saad Yusuf Saad alisema kuwa uchaguzi wa Agosti nane ulikumbwa na wizi wa kura na haukuwa wa haki na uwazi.Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatatu, Jaji Thande Mugure alisema kuwa kesi hiyo imekiuka kanuni za kesi za uchaguzi kwa mujibu wa katiba.Jaji Mugure alisema kuwa mlalamishi Saad alikosa kuchapisha kesi hiyo kwenye gazeti kwa mujibu wa katiba.“Mlalamishi ambaye ni mpiga kura alikosa kuchapisha kesi hii kwenye gazeti, hii ikiwa ni kinyume cha sheria za uchaguzi,” alisema Thande.Aidha, Jaji huyo alimkosoa Saad kwa kumkabidhi mtoto wa Mohammed mwenye umri wa miaka minane nakala za kesi hiyo, hatua ambayo ni kinyume cha sheria. “Saad alimkabidhi mtoto wa Aisha nakala za kesi hiyo badala ya kumkabidhi Aisha mwenyewe. Hii ni kinyume cha sheria,” alisema Thande.Mahakama imemuagiza Saad kulipa fidia ya shilingi milioni tatu kugharamikia kesi hiyo.Ombi hilo la kutaka kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo liliwasilishwa mahakamani wiki iliyopita na wakili Paul Butti anayemwakilisha Mohammed.Butti aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo haijatimiza vigezo muhimu vya kesi za uchaguzi kwa mujibu wa katiba.Wakili huyo alisema kuwa kesi hiyo inafaa kutupiliwa mbali kwa sababu haina sahihi ya mlalamishi, ambayo ni moja wapo ya kanuni ya kesi za uchaguzi.Butti aidha alisema kuwa kesi hiyo haijaweka wazi kura alizopata kila mgombea aliyeshiriki katika uchaguzi huo wa Agosti 8.Hata hivyo, Mwaniki Gitai, wakili anayemwakilisha Saad aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo imetimiza vigezo vyote vinavyohitajika kwenye kesi za uchaguzi, kinyume na inavyodaiwa na Butti.Mwaniki ameitaka mahakama kutupilia mbali ombi hilo na kumtaka Jaji Mugure kusikiliza kesi hiyo ili haki ipatikane kwa mteja wake.