Kesi ya kupinga mbinu zilizotumika katika kuorodhesha majina ya watu wanaopania kujaza nafasi ya jaji mkuu pamoja na naibu wake ilifanyika katika Mahakama kuu ya Mombasa siku ya Jumanne.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kesi hiyo ilisikizwa na Jaji George Odunga akiwa jijini Mombasa, kwa kuwa majaji wote nchini wanahudhuria kongamano jijini humo.

Ikumbukwe Yash Pal Ghai na wenziwe wawili wanaitaka Tume ya JSC kutupilia mbali majina waliyoyaorodhesha ya watakao jitosa kwenye kinyang`anyiro cha kumtafuta jaji mkuu na naibu wake.

Kupitia wakili wao Njoroge Wanyoike, wawili hao walisema kuwa JSC haikufuata sheria katika kuorodhesha majina hayo.

Aidha, wameitaka mahakama kuweka wazi kumbukumbu zilizotumika katika kuchagua wawaniaji hao.

JSC, kupitia wakili wao Njoroge Regera iliiambia mahakama kuwa tume hiyo ilifuata sheria na katiba katika mchujo huo.

Aidha, Regera aliongeza kuwa kamwe JSC haiwezi kutoa kumbukumbu hizo, kwa kuwa zitabakia kuwa siri kwa tume hiyo.

Shughuli ya kuchagua majaji wa mahakama ya juu akiwemo jaji mkuu inatarajiwa kuanza Agosti 29, mwaka huu.