Mahakama ya Mombasa imeahirisha kutoa uamuzi iwapo kesi ya ufisadi na utumizi mbaya wa afisi inayomkabili mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa itaendelea kusikilizwa katika mahakama ya Mombasa ama kuhamishwa hadi mahakama ya Lamu.
Hii ni baada ya uamuzi huo kutokuwa tayari siku ya Jumatano.
Mahakama itatoa uamuzi huo Machi 2, 2016.
Hatua hii inajiri baada ya mbunge huyo kuwasilisha ombi katika mahakama ya Mombasa mwezi uliopita kutaka kesi hiyo kusikilizwa katika mahakama ya Lamu kwa mujibu wa katiba, ikizingatiwa tukio hilo lilifanyika Lamu wala si Mombasa.
Mwezi uliopita wakili wa washtakiwa Gerad Magolo, aliambia mahakama kuwa kesi hiyo haipaswi kusikilizwa katika mahakama ya Mombasa ikizingatiwa tukio hilo lilitokea katika kaunti ya Lamu.
Magolo alisisitiza kuwa kesi hiyo inafaa kusikilizwa katika Mahakama ya Lamu ilikutoa nafasi kwa wakazi wa Lamu kuhudhuria vikao vya kesi hiyo ikizingatiwa wao ndio waathiriwa wakubwa.
Ombi lililokuwa limepingwa vikali na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexendra Muteti kwa kusema kuwa Mahakama ya Mombasa ina uwezo kikatiba kusikiliza kesi hiyo.
Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa na wanakamati 6 wa hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF wanatuhumiwa kutumia vibaya shilingi milioni 1.6 zilizokuwa zimetengewa ujenzi wa kituo cha kutibu mifugo eneo la Witu.