Jaji Anyara Emukhule ameafiki kuahirisha kesi ya uteuzi wa makamishna wa Tume ya Wakfu nchini, baada ya wakili Yusuf Abubakar na wenziwe kuomba muda wa wiki mbili ili kujitayarisha kwa kesi hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakili Abubakar amemtaka Jaji Emukhule kuahirisha kesi hiyo iliowasilishwa mahakamani na aliyekuwa Kadhi mkuu wa Kenya Sheikh Hammad Kassim, pamoja na viongozi wengine wa dini.

Viongozi hao waliishtaki afisi ya mkuu wa sheria Githu Muigai kuhusu uteuzi wa makamishna wa tume hiyo, huku wakitaka jaji huyo kusimamisha kutekelezwa kwa uteuzi huo hadi mahakama ifanye uamuzi.

Sheikh Kassim aliwasilisha kotini kesi hiyo akidai kuwa ofisi ya mkuu wa sheria imeenda kinyume cha katiba kwa kutohusisha jamii ya dini ya Kiislamu kabla ya kutekeleza uteuzi huo.

Hatua hiyo inahofiwa kugawanya waumini wa dini ya Kiisalamu hasa katika ukanda wa Pwani na nchi nzima kwa jumla.

Baadhi ya viongozi walioteuliwa na mkuu wa sheria ni Sheikh Juma Ngao, Dkt Mwanakitini Bakari ,Prof Hamadi Boga, Noor Zubeir Hussein, Nagib Shamsan na Shariff Hussein Ahmed.

Hapo awali, Sheikh Juma Ngao alitoa hisia kali juu ya swala hili huku akishtumu upande wa walalamishi kwa madai ya kuleta ubaguzi katika uongozi wa tume hiyo, kwa kutaka jamii fulani isalie madarakani.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tarehe Julai 28, mwaka huu.