Mahakama kuu ya Mombasa imetupilia mbali ombi la kutaka kesi ya wasichana wanne wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi kusikizwa na jopo la majaji watatu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akitoa uamuzi huo, Jaji Dora Chepkwonyi alisema kuwa kesi hiyo haina uzito wowote wa kuiwezesha kusikizwa na jopo la majaji watatu.

Jaji Chepkwonyi ameagiza kesi hiyo kuendelea kusikizwa katika mahakama ya chini ya Mombasa.

Haya yanajiri baada ya wasichana hao kupitia kwa wakili wao Hamisi Mwadzogo, kuwasilisha ombi la dharura mwezi Disemba wakiitaka Mahakama kuu kuteua jopo hilo ili haki na usawa kupatikana.

Mwadzogo alisisitiza kuwa kufikia sasa, upande wa mashataka unajikokota katika kuendesha kesi hiyo, jambo alilolitaja kama ukandamizaji wa haki za wateja wake.

Hii ni baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kutaka kuwafungulia mashtaka mapya wasichana hao baada ya mahakama kuwaachilia kwa dhamana.

Wanne hao ni Ummulkheir Abdullah kutoka Zanzibar mwenye umri wa miaka 21, Mariam Said Aboud pamoja na Khadija Abubakar wenye umri wa miaka 19 wote kutoka Malindi wanaodaiwa kuwa wanafunzi walioahidiwa ufadhili wa kimasomo nchini Somalia, na Halima Aden aliyekamatwa katika Kaunti ya Machakos kwa tuhuma za ugaidi.