Kesi ya ugaidi inayowakabili wasichana wanne imepata hakimu mpya atakaye isikiliza baada ya Hakimu Simon Rotich kujiondoa.
Siku ya Alhamisi, Hakimu Henry Nyakweba aliahidi kusikiliza kesi hiyo kwa haraka ili haki ipatikane.
Hatua hii inajiri baada ya Hakimu mkuu Teressia Matheka kutoa agizo la kumtaka Hakimu Nyakweba kusikiliza kesi hiyo.
Wakati huo huo, mahakama imedinda kuhamisha kesi hiyo hadi katika Mahakama ya Shanzu.
Haya yanajiri baada ya Hakimu Simon Rotich kujiondoa kwenye kesi hiyo wiki iliyopita na kusababisha kulemaa kwa kesi hiyo.
Hii ni baada ya maafisa wa kupambana na ugaidi ATPU pamoja na afisi ya mwendesha mashtaka ya umma kuwasilisha ombi la kumuondoa hakimu huyo.
Wiki iliyopita, Hakimu Simon Rotich alisisitiza kuwa juhudi zake za kufanikisha kesi hiyo kusikilizwa kwa haraka ndio chanzo cha kutakiwa kujiondoa katika kesi hiyo.
Washtakiwa Maryam Said Aboud, Ummulkheir Sadri Abdalla, Khadija Abubakar Abdulakadir na Halima Adan wanadaiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la al-Shabaab baada ya kutiwa mbaroni mwaka jana katika eneo la Elwak huko Mandera.