Hatua ya Wizara ya Usalama kupunguza idadi ya walinzi wa Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho na Gavana wa Kilifi Amason Kingi inazidi kuibua hisia mbalimbali nchini.
Kwenye kikao na waandishi wa habari afisini mwake siku ya Jumatano, Katibu Mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, alisema kuwa anaunga mkono hatua hiyo.
Khalifa alitaja kupunguzwa kwa idadi ya walinzi wa viongozi kama hatua nzuri inayofaa kutekelezwa kwa kila kiongozi nchini, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa ulinzi wa kutosha badala ya watu wachache kunufaika.
“Hawa viongozi wakati mmoja walikuwa wananchi. Leo hii wanataka walindwe na maafisa wa polisi zaidi ya 10. Mkenya asiye na mlinzi hata mmoja haki yake iko wapi? aliuliza Khalifa.
Aidha, kiongozi huyo wa kidini aliihimiza serikali kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi anayepewa zaidi wa walinzi watatu, ili maafisa wengine wa kulinda usalama wapelekwe katika maeneo ambayo hali ya usalama imedodora.
Kauli ya Khalifa inajiri wiki moja tu baada ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kupokonywa walinzi wake na idara ya usalama kwa madai kuwa walinzi hao wanapelekwa kupata mafunzo zaidi.