Ukosefu wa mvua unaoshuhudiwa umetishia mazao ya kilimo kulingana na wakulima wa eneo la Gachuba.
Kulingana na wakulima hao, hali hii ikiiendelea huenda hata mimea ikakosa kunawiri au ikakauka na baadhi ya mifugo ata kuangamia, kwani hali inazidi kuwa mbaya zaidi.
Mvua ilinyesha mwisho wa mwezi wa Januari, jambo ambalo limepelekea wakulima hao kuhofia hali ya mimea na mifugo wao.
Wakulima wa eneo hilo la Gachuba ambao wengi ni wapanzi wa chai, mahindi na maharagwe hutegemea sana kilimo ili kujiendeleza kimaisha, na hata kukimu mahitaji ya wanao shuleni.
Ingawa baadhi ya mimea imeonyesha dalili za kukauka, wengi wana matumaini kuwa huenda ikanyesha hivi karibuni huku wengine wakilichukulia swala hili kuwa badiliko la anga na misimu na ongezeko la uchafu katika anga kutokana na shughuli za kila siku za binadamu.
Baadhi ya wakulima ambao wamepanda mimea ya vipindi vifupi wamelazimika kunyunyizia mimea yao maji ili izidi kunawiri.
Wakulima hao hulazimika kuchota maji kutoka mito iliyoko karibu ambayo hushuhudia foleni ndefu za watu walio kwa harakati za kupata angalau tone wasaidie mimea yao.