Spika wa bunge la kaunti ya Nakuru Susan Kihika amewataka wakenya kuwaombea na kuwasaidia mayatima nchini pamoja na waadhiriwa wote wa dhuluma za kijinsia.
Katika ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa Facebook siku ya jumatatu, Kihika alielezea kusononeka kwake baada ya mauaji ya wikendi iliyopita ya Olivia Osidiana, mama wa watoto wawili.
Osindina mwenye umri wa miaka thelathini na sita, anadaiwa kuuawa na mumewe ambaye walikuwa wametengana naye siku ya jumamosi kwa kudungwa kisu mara kadhaa mwilini katika nyumbani mwao kwenye mtaa wa Freehold mjini Nakuru.
Hatimaye mwanaume huyo ambaye polisi walimtambua kama Jack Omondi alijitia kitanzi baada ya kisa hicho.
Katika kile kinaonekana ni kuandamwa na mkasa baada ya mwingine, Osindina aligonga vichwa vya habari baada ya kuzuiliwa kwa miezi kadhaa mapema aprili mwaka huu kwenye hospitali ya War Memorial mjini Nakuru, baada ya kujifungua mtoto Jeremy lakini akashindwa kulipa bili iliyofikia zaidi ya shilingi elfu mia tano.
Serikali ya gavana Kinuthia Mbugua ilitoa fedha kwenye mfuko wa dharura na kumlipia mama huyo deni hilo, huku spika Kihika akiongoza ujumbe ulioenda kumnusuru mama huyo.
“Ninahuzunika moyoni ninapokumbuka machozi ya furaha aliyokuwa nayo (mama Jeremy) alipojua kwamba hatimaye angempeleka mwanawe nyumbani…” alisema Kihika kwenye ukurasa huo.
Aliendelea kusema: “Ninaomba wakenya kuwaombea watoto wawili aliowaacha pamoja na wanaodhulumiwa katika jamii tukiadhimisha siku kumi na sita za kupigana na dhuluma dhidi ya wanawake na watoto”.
Hata hivyo alisema wakati umefika kwa wahalifu kutolindwa tena, ila kulinda wananchi kutodhulumiwa na kuhangaishwa tena.
“Ninaona wengi wa hawa wahalifu wakitembea na adhabu kidogo tu hata baada ya vitendo vyao vya kihalifu,” spika aliongezea.
Omondi, ambaye alikuwa mfanyikazi katika kampuni moja ya Nakuru, alikuwa ametengana na mkewe huyo kwa muda mrefu, na mauaji hayo yametokea majuma kadhaa baada ya wao kurudiana.