Familia moja katika kijiji cha Monga, wadi ya Nyamaiya, inaendelea kuomboleza kifo cha mwanao.
Kijana huyo wa miaka 23, anadaiwa kunywa sumu baada ya kukatazwa na mamake kumchumbia msichana fulani katika eneo hilo.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumapili, naibu chifu wa kata ndogo ya Bomanyanya Joseph Mongare alisema kuwa kwa muda sasa, kijana huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu kwenye Shule ya upili ya Mageri hajakuwa akilipa karo ya shule kwa kuwa amekuwa akitumia karo hiyo kumfurahisha mpenziwe.
"Kwa muda sasa mwendazake hajakuwa akilipa karo ya shule ambayo mamake amekuwa akimpa kwa kuwa amekuwa akimpa mpenziwe pesa hizo,” alisema Mongare.
Mongare aidha alisema kuwa jamaa wa kijana huyo walijaribu kuokoa maisha yake lakini hawakufanikiwa.
"Familia ya marehemu ilijaribu kumwokoa na kumpeleka katika Hospitali Kuu ya Nyamira kupokea matibabu lakini akaaga dunia pindi tu alipofikishwa hospitalini,” alisema Mongare.
Kwa sasa mwili wa kijana huyo unahifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Kuu ya Nyamira.