Huku Wakenya wakizidi kulalamikia hali ngumu ya maisha kwa madai kuwa hali ya uchumi iko juu, kutana na jamaa aliyeamua kutafuta riziki kwa kutengeneza zulia kutumia kamba zilizotupwa.
Keneddy Otieno, mwenye umri wa makamo na ambaye ni mkaazi wa Mtongwe mjini Mombasa, aliamua kujihusisha na biashara ya kutengeza zulia za mlangoni kwa kutumia kamba za makonge zinazotupwa baada ya kutumika.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi katika kibanda chake kilichoko karibu na kivuko cha feri, Otieno alisema kuwa yeye hurauka kila asubuhi na kuenda kwenye vibanda vya kuuzia mboga ili kuokota kamba hizo, kabla ya kuanza rasmi kusuka zulia hizo.
“Napata kamba hizi bure kutoka kwenye sehemu za kutupa takataka. Mara ya kwanza watu walidhani mimi ni mwendawazimu lakini saa hii wanakuja kibandani kwangu kununua zulia,” alisema Otieno.
Otieno mwenye vipawa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchoraji, alisema kuwa amekuwa akihangaika kutafuta kazi kwa muda mrefu bila mafanikio, kabla ya kugutuka na kugundua kuwa kipaji chake kinaweza kumnufaisha pakubwa.
Alisema kuwa kwa sasa kipaji chake kinamtimizia mahitaji yake muhimu.
“Kabla ya kuanzisha biashara hii, nilikuwa nikiuza miraa lakini nikaona ni njia moja ya kupotosha vijana. Sikufurahia vile ambavyo vijana wadogo walikuwa wakija kununua miraa,” alisema Otieno.
Aidha, Otieno anayejipatia mapato kwa kuuza zulia moja kati ya shilingi 300 hadi 400, amewasihi vijana kujihusisha na kazi mbalimbali ili kujiendeleza kimaisha.
Alisema kuwa kila kijana yuko na kipaji na cha muhimu ni kukigundua na kukitumia vizuri.