Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Tarehe 4 mwezi Februari kila mwaka watu wa matabaka mbalimbali ulimwenguni hujumuika pamoja katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani kama njia moja ya kutoa hamasisho dhidi ya maradhi hayo hatari.

Kama ilivyo desturi, ulimwengu ulijumuika pamoja Alahamisi hii kuadhimisha siku hiyo huku watu wote wakihimizwa kutembela vituo vya afya kukaguliwa.

Huku hayo yakiendelea, kijana mmoja mjini Mombasa aliamua kujitolea na kujiunga na mashirika mbalimbali kuhamasisha umma.

Guga Ramadhan ana umri wa miaka 21, na akiwa bado katika shule ya upili alimpoteza mamake mzazi mwaka wa 2011 kutokana na ugonjwa wa saratani ya matiti.

Akoongea na mwandishi huyu, Ramadhan alieleza jinsi maisha nyumbani yalivyokuwa magumu pamoja na shuleni kwani mamake ndiye aliyekuwa akitegemewa.

“Kwanza hata alipoanza kuugua mambo yalikuwa magumu kwa sababu pesa zote zilitumika kwa matibabu, alafu alipofariki hapo ndipo mambo yalivurugika zaidi.’’ Alieleza Ramadhan.

Baada ya kumaliza ya kumaliza masomo yake kupitia msaada kutoka kwa wahisani, kijana huyu aliamua kujitosa katika vita dhidi ya maradhi haya ambayo yalimpokonya mzazi tegemezi.

Alijisajili katika kituo cha kuwashughulukia wagonjwa sugu cha Coast Hospice kama mfanyikazi wa kujitolea ambapo hujishughulisha na kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na kushiriki katika hafla mbalimbali za kuhamasisha umma dhidi ya saratani mkoani pwani.

“Uwa nasikitika sana nikimkumbuka mamangu mzazi na pia nafahamu kwamba wapo watoto wengi wasio na wazazi kutokana na saratani, nimechukua fursa hii kusaidia jamii ili niwanusuru wenzangu pia.” Aluiongeza Kijana huyo.

Ramadhan pia ni mtunzi wa nyimbo na mashairi na hutumia kipaji hicho kuandika mashairi ya kutoa hamasisho katika jamii ambapo pia aliandika shahiri la kumuenzi marehemu mama yake.

Kulingana na shirika la afya duniani, asilimia 13 ya vifo duniani husababishwa na saratani huku visa vingi vikiripotiwa katika mataifa yenye kipato cha chini, na Ramadhan anaeleza matumaini ya juhudi zake kuleta mabadiliko.