Kijana anayedaiwa kumjeruhi afisa wa usalama pamoja na kumnyang’anya bunduki yake amesomewa mashtaka upya katika Mahakama ya Mombasa.
Mshukiwa, Jackson Kimau, pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani wanadaiwa kumnyang’anya afisa huyo, Kikuyu Jarson, bunduki aina ya AK47, risasi 30, pamoja na kumjeruhi huku wakiwa wamejihami kwa silaha hatari.
Vijana hao wanadaiwa kutekeleza kitendo hicho mwezi Mei mwaka jana katika eneo la Changamwe.
Upande wa mashtaka ulisema siku ya Jumatatu kuwa sababu ya kusoma upya mashtaka ni kubadilisha nambari ya bunduki walionyang’anya afisa huyo.
Hakimu Susan Shitubi alimwelezea mshukiwa kuwa ni haki yake kuwaita shahidi waliotoa ushahidi hapo awali, kwa sababu amesomewa mashtaka hayo upya.