Idara ya Polisi eneo la Pwani imewahakikisha wakaazi usalama dhabiti.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamanda mkuu wa Polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi amesema kuwa wametuma maafisa wa usalama katika kila eneo ili kukabiliana na wahalifu wanaolenga kuwahangaisha wakaazi.

Wanjohi alisema kuwa idara hiyo imeeandaa mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa usalama wa Pwani unaimarishwa, huku akisema kuwa atakayepatikana akipanga njama ama kuwahangaisha wakaazi atakabiliwa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Wanjohi alisema kikosi maalum cha kukabiliana na magaidi na wahalifu kimetumwa mashinani kuchunguza na kuwakabili vikali wahalifu wanaowavamia wakaazi na kuwaua bila sababu zozote.

"Tumetuma kikosi maalum kulinda usalama wa wakaazi wetu na kuhakikisha kuwa inakabiliana kikamilifu na watu wanaolenga kuvurugu usalama wa wananchi,” alisema Wanjohi.

Kauli ya Kamanda huyo mkuu wa Polisi eneo la Pwani imejiri siku moja tu baada ya watu watatu kupigwa risasi na kuuawa katika hali ya kutatanisha katika kijiji cha Bongwe-Gombato eneo la Ukunda Kaunti ya Kwale.