Naibu Spika wa Bunge la Kaunti ya Nyamira Andrew Magangi asema kuwa kilimo cha kahawa katika eneo la Gusii chafaa kupewa kipau mbele hasa katika Kaunti ya nyamira.
Naibu Spika Magangi alisema haya siku ya Jumamosi alipokuwa katika eneo la Ikonge akiwa kwenye harakati na juhudi zake mwenyewe kuafikia lengo lake la kuhimiza wakulima hasa vijana wa Kaunti hiyo kuingilia kilimo cha kahawa.
kulingana na Magangi, kilimo cha kahawa kimekuwa na mikosi yake kwa wakulima na kuongeza kuwa njia mbadala ya kuokoa hadhi ya kilimo katika Kaunti ya Nyamira yafaa kutafutwa, ambayo alisema ni kilimo cha kahawa.
“Kilimo cha majani chai kimewaweka wakulima kwenye mateso ya kutopokea hela za kutosha huku baksishi zao zikiendelea kudidimia kila kuchao na hatuwezi kukimya kwa hilo,” alisema Magangi akisisitiza kuwa atayaalika mashirika ya kufadhili kilimo cha kahawa ili wakulima wawe vyema.
Aidha wakulima waliojitokeza walionekana kufurahia jambo hilo huku wakitaka Kaunti hiyo iwe ya kwanza kuimarisha kilimo cha kahawa kando na vyakula vingine vilivyokuwa hapo awali ambapo walikuwa wakipokea faida ya hela nyingi kutokana na mishahara na marupurupu mengine kutokana na kahawa.
Wakati uo huo Magangi alisema kuwa kwa sasa wakulima watakuwa macho kulinda mali yao kutoka mikononi mwa wasimamizi na wakuu wa almashauri ambao katika siku za hapo awali walinyakua na kuyauza mashamba ya hisa waliowekeza wakulima hao.