Wakulima katika kaunti ya Nakuru walipokea zaidi ya Sh14 bilioni kutokana na mauzo ya lita 291,275,413 za maziwa mwaka jana, kulingana na rekodi za idara ya mifugo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Uzalishaji wa maziwa ulipanda kwa asilimia 0.3 kutoka mwaka 2013, jambo ambalo limeipa serikali ya kaunti msukumo kubuni mbinu mpya zinazolenga kuimarisha uzalishaji wa zao hilo.

Gavana Kinuthia Mbugua hivyo basi amewahakikishia wakulima kwamba serikali yake imebuni mikakati ya kuzidi kuinua sekta hiyo.

Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na afisa wa mifugo Virginia Ngunjiri, wakati uzinduzi wa mradi wa India-Kenya Dairy Innovation Programme (IKDIBP) mjini Nakuru unaolenga kuimarisha sekta ya ukulima wa maziwa, gavana Mbugua alisema serikali ya kaunti itajenga vituo vya kuhifadhi maziwa katika wilaya zote 11 za kaunti hiyo.

“Wakulima wametambua kuna pesa katika ukulima wa maziwa na jukumu letu ni kuwasaidia kuendeleza na kuimarisha kilimo chao. Vituo vya kuhifadhi maziwa vitasaidia kupunguza hasara kutokana na kuharibika kwa maziwa,” alisema gavana Mbugua.

Mbugua alifichua kwamba serikali ya kaunti ilitenga Sh33.7 katika kipindi cha 2014/2015 kwa kuinua ufugaji katika eneo hilo huku akikariri umuhimu wa kuimarisha kilimo cha maziwa ili kubuni nafasi za kazi na kupunguza makali ya njaa.

Wakati huo huo gavana Mbugua alisema kwamba uzalishaji wa maziwa katika kaunti ya Nakuru unazidi utumiaji wa zao hilo jambo alilosema limepelekea kuanzishwa kwa kampeini za kuwarai wakazi wa Nakuru kukumbatia unywaji wa kila mara wa maziwa.

“Serikali ya kaunti itasaidia viwanda vya maziwa kutengeneza bidhaa ambazo zinavutia hasa vijana kama njia mojawapo ya kuinua matumizi ya bidhaa zinazotokana na maziwa,”alisema Mbugua.

Mradi wa IKDIBP,  ambao unaendeshwa na shirika la maendeleo Duniani (USAID) unalenga kuongeza uzalishaji wa maziwa,usimamizi wa sekta ya maziwa na uimarishaji wa utengenezaji wa bidhaa za maziwa ili kuongeza mapato ya wakulima.

Kulingana na ripoti ya idara ya mifugo,maeneo ya Kuresoi Kaskazini ,Kuresoi Kusini na Bahati ndiyo yaliyoongoza katika uzalishaji wa maziwa katika kaunti hiyo mwaka jana.

Vilevile ilidhihirika kwamba mauzo ya maziwa kupitia vyama vya ushirika yaliongezeka jimboni.