Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa maswala ya vijana na taasisi za kiufundi katika Kaunti ya Nakuru amesema serikali ya kaunti inafanya kazi kwa pamoja na makundi yanayowashughulikia watu wanaoishi na ulemavu ili kuboresha maisha yao.

Akizungimza na mwandishi huyu kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumatatu, Josphat Kimemia, alisema kuwa kufuatia kufanya kazi pamoja na makundi hayo, serikali ya Kaunti ya Nakuru imeweza kubaini idadi ya watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti hiyo.

Aidha, Kimemia alisema kwamba kuna kitengo cha kushughulikia watu wanaoishi na ulemavu kwenye kaunti ya Nakuru ambacho kina mkurugenzi wake ambaye ametauliwa na Gavana Kinuthia Mbugua.

Alisema kuwa lengo la kitengo hicho ni kushughulikia mahitaji ya watu wanaoishi na ulemavu.

Kimemia alisema kitengo hicho ambacho pia kina wajibu wa kushughulikia wazee na watoto wanaorandaranda mitaani, kina bajeti yake ya kukiwezesha kuendeleza shughuli zake.

Kwa upande mwingine, aliangazia swala la watoto wanaoishi na ulemavu akisema kuwa kwa miaka mingi, kundi hilo la watoto limekuwa likitengwa.

Kulingana naye, kundi hilo pia limekuwa likinyinwa haki ya kuonekana na pia kusikika kwa miaka mingi.

Kutokana na hilo, amewataka wakaazi wa Nakuru na Wakenya kwa jumla kulikumbatia kundi hilo akisema watoto hao ni wazalendo kwa njia moja au nyingine.