Kikundi kimoja cha akina mama katika mtaa wa Sewage mjini Nakuru wamejiandaa kutoa kanda ya video kuhusu adhari za pombe haramu.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akina mama hao wanaongozwa na Elizabeth Wanjiku, ambaye ni kinara wa wafanya kazi wa afya wa jamii (Community Health Workers). Wanasema wataonyesha vile pombe hutayarishwa katika mazingira chafu na adhari zake kwa wanayoibugia na jamii yote kwa jumla.

“Eneo hili letu ni ndogo sana lakini viwanda vya pombe ni vingi sana,” anasema Elizabeth. Anaongeza kwamba hadi sasa, wagema watatu wamesajirisha biashara zao lakini historia yao sio nzuri.

“Hatuwazuii watu kufanya biashara na kutengeneza ajira lakini hawa watu tumewajua tangu jadi na mbinu zao tunazielewa,” anaendelea kulalamika.

Hata hivyo, wanaowatia kinyongo zaidi akina mama hawa na wale wanaouza pombe kwenye ploti.

“Katika filamu yetu, tunataka kuangazia mazingira yanayowaadhiri watoto ambao huzaliwa humu kupitia mienendo na matamshi ya walevi. Tunataka pia kumulika jinsi ulevi huadhiri familia na pia mazingira chafu ya kutengenezewa pombe hii,” Elizabeth anaendelea kuongeza.

Mtaa wa Sewage katika wadi ya Rhonda una walevi wengi sana na akina mama wengi wameunga mradi huu mkono. Wengi wamejitolea kushiriki katika filamu hiyo na kila mmoja ana malalamishi yake kuhusu pombe hii.

“Bwanangu alipotelea kwa mama pima na vijana wangu wamemfuata. Kama filamu hii itaweza wengine ambao walikuwa nia ya kuwa walevi, niko tayari kujitolea kwa hali na mali kunufaisha mradi huu,” anasema mama anayejitambulisha kama mama Maina.