Kina mama katika kaunti ya Kisii wanalalamikia kutengwa na kubaguliwa na mipangilio maalum kuhusu uendelezi wa kaunti.
Haya yalijitokeza jana wakati wa sherehe za Madaraka, ambapo mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake eneo bunge la Nyaribari Chache Clare Ondari aliitwa kutoa hotuba yake katika uga wa Gusii.
Kulingana naye, sheria za kufuatwa kwa msingi wa katiba hazijakuwa zikifuatwa vilivyo, na hakuna mpangilio wa jinsi jinsia ya kike ingejihusisha moja kwa moja na sherehe hiyo kwani hawakufahamishwa kama viongozi ila walikuja kushuhudia tu.
“Tunazungumzia kuzingatia uwakilishaji sawa ama hata thuluthi moja ya uhusisho ambao hatujaona hapa hata kwa makundi ya utumbuizaji, ilhali tumewekewa viti mbali na wageni wa heshima,” alisema mama huyo, ambaye pia aliunga mkono dhana ya serikali kuutambua usawa wa uwakilishaji ambao sasa utambuzi umekuwepo.
Aliwataka kina mama kutojidharau na kujitokeza ili kuwania nyadhifa mbalimbali ili kuweka upinzani bora na uongozi mbadala kwa kina mama wanao maono na hisia za wapiga kura kwa roho, kando na wenzao wa kiume.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae, naibu wake Joash maangi, na wabunge kando na viongozi wengine.