Share news tips with us here at Hivisasa

Makundi ya wanawake walemavu kutoka kaunti ya Mombasa wameamua kuungana pamoja na kushinikiza serikali ya kaunti kuzingatia sheria katika uteuzi wa wawakilishi wa walemavu bungeni.

Wanawake hao wanasema kuwa licha ya kwamba katiba imetoa nafasi ya uwakilishi wa walemavu bungeni, kumekuwa na ufisadi katika uteuzi huo katika kaunti hiyo, ambapo ni mwakilishi mmoja tu aliyeteuliwa katika bunge hilo.

Akiongea wakati wa kikao cha pamoja katika ukumbi wa Kongowea siku ya Jumatano, katibu wa mipango katika kikundi cha wanawake walemavu eneo hilo Bi Lucy Chesi alisema kuwa anasikitishwa na jinsi wanawake wameachwa nyuma.

“Mwakilishi aliyeteuliwa katika kaunti ni mmoja tu tena ni mwanaume na hakuna hata mwanamke mmoja, hiyo inawakosesha walemavu haki yao kwa sababu ni kinyme cha sheria,” Alisema Chesi.

Wanawake hao wanadai kwamba walemavu wanapitia changamoto nyingi huku wakiongeza kwamba wanawake ndio wenye matatizo mengi ikilinganishwa na wanaume na hivyo wanapaswa kuwakilishwa ipasavyo bungeni.

Wakati huo huo makundi hayo ya walemavu yamewasihi wenzao kuungana na kuongea kwa sauti moja kwani kumekuwa na madai kwamba walemavu wengi uwa hawafuatilii maswala yanayowahusu.

Kwa upande wake mwakilishi wa kipekee wa walemavu katika bunge la kaunti Hudson Karume alikiri kwamba kuna tatizo katika utekelezwaji wa sheria ambapo walemavu wa kike walinyimwa nafasi hiyo muhimu.

Karume alisema kuwa wakati wa uteuzi huo kulikuwa na ufisadi huku akiongeza kwamba iliwabidi waelekee kortini ili yeye akapata nafasi hiyo.

“Katika serikali hii ya kwanza kumekuwa na balaa nyingi sana jambo lililofanya mpaka tukaeleka kortini mimi nikiwa mmoja wao na ndio maana mnaona hali hii ambapo akina mama hawajaweza kuwakilishwa,” alisema Karume.

Wakati huo huo karume aliongeza kwamba kuna haja ya akuongezwa mwakilishi mwingine kwani majukumu anayotekeleza ni mengi mno na hivyo anahitaji mtu wa kushirikiana naye.

Picha: Watu wenye ulemavu kwenye hafla katika picha ya awali. Makundi ya walemavu kaunti ya Mombasa yanaitaka serikali ya kaunti kuzingatia sheria wakati wa kuteuwa wawakilishi wa walemavu bungeni. The-star.co.ke