Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kina mama kutoka kaunti ya Nyamira wamehimizwa kujiunga na vyama vya kisiasa ili kuwania nyadhifa mbalimbali za serikali kama njia mojawapo yakuingia mamlakani.

Akihutubia kina mama Nyansiongo baada ya hafla ya kuchangisha pesa za ujenzi wa kanisa la kiadventista la Menyenya, seneta mteule Daisy Nyongesa alisema kuwa kina mama wamekuwa na changamoto za kushikilia nyadhifa za uongozi kwa kuwa wanaume huwapiku kwenye chaguzi mbalimbali.

“Kuwa na mahusiano ya karibu na vyama vya kisiasa ni njia mojawapo ya kutusaidia sisi kina mama kuingia afisini, na kunyamaza kwetu ndiko kunacho sababisha tusichaguliwe, na sasa wakati umewadia kwetu kina mama kujitokelea kuchangia kwenye masuala mbalimbali ya chama," alisema Nyongesa.

Seneta huyo aidha aliwapa changamoto kina mama kupigania nyadhifa mbalimbali kwenye chama cha ODM badala ya kungojea kupewa uteuzi wa moja kwa moja.

" Wengi wetu tulijitolea kwa shughuli nyingi za chama cha ODM na ndio maana tuliteuliwa na ni jambo zuri chama cha ODM kikiwa na kina mama watakaojitokeza kuwapinga wanaume kwenye nyadhifa mbalimbali,” alihimiza Nyongeza.

Seneta huyo aidha alisema kuwa kutotekelezwa kiukamilivu usawa wa jinsia kwenye nyadhifa mbalimbali ni mambo ambayo yanafaa kuwa ya kitambo, iwapo tu wanawake wangejitokeza kuchangamkia siasa na shughuli za vyama vya kisiasa.