Vikundi vya akinamama na Vijana kutoka maeneo Bunge mbali mbali katika Kaunti ya Kisii wameukumbatia mradi wa Serikali Kuu kwa kutoa mikopo mbali mbali kwao ili kujiendeleza kimaisha na kuinua viwango vya uchumi na maendeleo.
Wakiongea siku moja tu baada ya Katibu Mkuu katika Wizara ya Ugatuzi na Mipangilio ya Serikali Ann Waiguru kuwatembelea na kutoa pesa kwa baadhi yao, Akinamama hao sasa wamepongeza hatua ya Serikali Kuu kwa kuwakumbuka na kusema kuwa wako tayari kwa funzo maalumu jinsi ya kupata na kutumia pesa hizo.
“Tuko tayari kwa funzo maalumu jinsi tutakapopata na kutumia pesa hizo ili kujiendeleza kimaisha na kuinua viwango vya maendeleo katika jamii zetu,” alihoji Priscah Nyanchoga mmoja wa wanachama cha kundi la Osweta.
Kwingineko kinamama hao wamewaomba kinamama ambao bado hawajajiunga na vikundi kufanya hivyo kwa kuwa kikundi ni njia mojawapo itakayowawezesha kupokezwa mikopo hiyo.
Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi naye alisema kuwa kinamama hao na Vijana wanahitaji funzo maalum kwa kuwa wengi wao hawajafahamu umuhimu wa kujiunga katika vikundi ili kupewa mikopo.
Angwenyi alitaja kina mama kuwa msingi wa uchumi wa nchi, bila wao uchumi wa Kenya hautaendelea na kuwaomba wote pamoja na Vijana kuendelea kufanya bidii katika kazi zao za kila siku ili kujiendeleza.
Pia Angwenyi aliipongeza Serikali Kuu kwa kuwakumbuka kinamama hao na kuomba Serikali ya Kaunti ya Kisii kushirikiana na ile ya kitaifa ili kuendeleza mradi huo.