Gavana wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi ameikosoa serikali kuhusiana na jinsi inavyoendesha uchunguzi dhidi ya wizi wa shillingi millioni 52 kutoka kwa hazina ya kaunti hiyo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia wanahabari huko Kilifi, Kingi alidai kuwa serikali imechelewesha uchunguzi katika kesi hiyo.

"Sijafurahishwa na jinsi uchunguzi unavyoendeshwa. Imechukua taasisi za kukabiliana na ufisadi muda mrefu kufanya uchunguzi, jambo ambalo litachelewesha hatua ya washukiwa kupelekwa mahakani na kukabiliwa na mkono wa sheria," alisema Kingi.

Hata hivyo, Kingi alisema kuwa ana imani kuwa fedha zilizoibiwa zitaregeshwa pindi wahalifu waliohusika watakapobainika.

“Kufikia sasa tumefungulia mashtaka watu 10, kampuni tano na benki nne, na tumepewa agizo akaunti za kampuni zilizohusika zisitumike hadi kesi itakapoisha. Kama wakuu wa Kaunti ya Kilifi, tutashirikiana na vitengo vya uchunguzi hadi pale pesa hizo zitakaporudishwa na waliohusika kupelekwa mahakamani," alisema Kingi.

Aidha, Kingi aliishukuru Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), kwa ushirikiano mwema na kuwahimiza kuendelea na kazi yao dhidi ya kashfa hiyo.