Mke wa gavana wa kaunti ya Nakuru Lucia Kinuthia sasa ameelekezea kidole cha lawama maafisa wakuu wa afya katika kaunti na kusema kuwa wamechangia pakubwa upungufu wa wauguzi.
Bi Kinuthia ambaye ameonekana kugadhabishwa na hatua hiyo ameonya kuwa upungufu huo huenda ukaleta shida kubwa ikiwa hatua na mipango mwafaka haitachukuliwa.
Amekasirishwa na hatua ya kuwepo kwa mhudumu mmoja kwenye idara ya wagonjwa wa ulemavu wa kiakili maarufu kama Celebral Palsy katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
"Ni jambo la kutamausha kuona muhudumu moja akishughulikia idadi kubwa ya wagonjwa pekee yake, kwani hatuna wasimamizi wa idara ya afya kwenye kaunti?" Kinuthia alisema.
Mnamo mwaka wa 2014, Bi Kinuthia alikuwa amezuru hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha na kuagiza kuwa idara hiyo iongezewe wahudumu zaidi tukio ambalo halikufanyika hadi wa sasa.
Alikuwa akizungumza Alhamisi baada ya kuzuru hospitali hiyo na kufanya kikao na maafisaa wakuu wa afya akiandamana na MCA wa eneo la Viwandani Eunice Mureithi.