Kiongozi wa dini ya Kiislamu ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 30, kwa kosa la kuhifadhi mshukiwa wa ugaidi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kupi Shee Kupi alitiwa mbaroni siku ya Jumanne wiki iliyopita katika eneo la Majengo, kwa madai ya kuhifadhi Ismail Shosi, mshukiwa wa ugaidi aliyeuawa na polisi siku kadhaa zilizopita.

Kupi hata hivyo, alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu mkuu Julius Nange'a.

Wiki iliyopita, Mahakama ya Mombasa ilimzuia Kupi kwa wiki moja, ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa uchunguzi.

Haya yalijiri baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kuomba muda zaidi wa kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo.

Mwendesha mashtaka Josphine Mwaura aliiambia mahakama kuwa uchunguzi wa kesi hiyo ni wa kina na unahitaji muda wa kutosha.

“Tunataka kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai haya, kabla ya kumfungulia mashtaka mshukiwa huyu,” alisema Mwaura.

Ombi hilo lilipingwa na wakili wa mshtakiwa, Yusuf Aboubakar, aliyesema kuwa mteja wake hana hatia yoyote bali hiyo ni njama ya kukandamiza haki zake za kibinadamu.