Kiongozi mmoja wa dini ya kiislamu amefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kwa tuhuma za kutoa hifadhi kwa mshukiwa wa ugaidi.
Kupi Shee Kupi alitiwa mbaroni siku ya Jumanne katika eneo la Majengo, kwa madai ya kuhifadhi mshukiwa wa ugaidi Ismail Shosi aliyeuawa na polisi wiki iliyopita.
Haya yanajiri baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashataka ya umma tawi la Mombasa kuomba muda zaidi wa kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo.
Mwendesha mashtaka Josphine Mwaura aliimbia mahakama kuwa uchunguzi wa kesi hiyo ni wa kina na unahitaji muda wa kutosha.
“Tunataka kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai haya, kabla ya kumfungulia mashtaka mshukiwa huyu,” alisema Mwaura.
Ombi hilo lilipingwa na wakili wa mshtakiwa, Yusuf Aboubakar, aliyesema kuwa mteja wake hana hatia yoyote bali hiyo ni njama ya kukandamiza haki zake za kibinadamu.
Hata hivyo, Hakimu Martin Rabera alikubali ombi hilo na kuagiza mshukiwa huyo kuzuiliwa kwa siku saba zaidi.