Kiongozi wa jamii ya Mijikenda Vincent Mwachiro ameipongeza serikali kuu kwa kutimiza ahadi yake ya kuwapa wanafunzi wa shule za msingi za umma fursa ya kupata masomo kwa mfumo wa kidijitali.
Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Ijumaa, Bw Mwachiro alisema kuwa ni afueni kuona kwamba hatimaye baadhi ya shule za msingi katika Kaunti ya Mombasa na baadhi ya maeneo ya Pwani zikifaidi na mradi wa serikali wa vipakatalishi.
“Ningependeza kupongeza serikali kwa kuanzisha mradi huu kwani utapiga jeki sekta ya elimu,” alisema Mwachiro.
Aidha, Mwachiro alipongeza baadhi ya shule zilizopokea vipakatalishi hivyo ikiwemo Shule ya msingi ya Spaki iliyoko mjini Mombasa.
Hata hivyo, aliwaomba viongozi kutotia siasa kwenye mradi huo, kwa kusema kuwa hali hiyo huenda ikasababisha sekta ya elimu kudorora.