Kiongozi wa walio wachache kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Jackson Mogusu amejitokeza kushtumu vikali vurugu iliyoshuhudiwa kwenye bunge la kitaifa wakati Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa akitoa hotuba yake kwa taifa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu Alhamisi jioni, Mogusu alisema kuwa ni aibu kwa wabunge wa muungano wa CORD kutomheshimu rais, hali aliyosema inaonyesha kutokomaa kwao kisiasa. 

"Ni aibu iliyoje kwa viongozi wa kitaifa kuvuruga hotuba ya Rais Kenyatta bungeni ikizingatiwa kwamba cheo cha urais ni ishara ya kuliunganisha taifa na kwa kweli hii ni ishara kwamba wabunge hao hawajakomaa  kisiasa," alisema Mogusu. 

Mogusu aidha aliongeza kwa kumtaka spika wa bunge la kitaifa kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wabunge waliohusika kwenye vurugu zilizotatiza hotuba ya rais kwa nusu saa, huku pia akiwataka wananchi kutowapigia kura viongozi wa aina hiyo. 

"Tabia ambayo baadhi ya wabunge wa mlengo wa CORD wameidhihirisha bungeni ni wazi kwa wakenya kwamba watu wa aina hiyo hawastahili kuwawakilisha wananchi bungeni, na ni ombi langu kwa spika Muturi kuwachukulia hatua za kinidhamu," aliongezea Mogusu.