Kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira amejitokeza kuitaka tume ya uchaguzi na mipaka IEBC kuupa mlengo wa CORD nafasi ya kuanzisha mchakato wa marekebisho ya rasimu ya Katiba.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumatano Masira alisema kuwa yafaa tume ya IEBC iupe mlengo wa CORD nafasi ya kurekebisha sahihi zilizokuwa na makosa.
"Naona kwamba ingekuwa kheri kwa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC kuruhusu mlengo wa CORD kufanyia marekebisho sahihi zilizokuwa na makosa ili kuruhusu muungano huo kusukuma agenda ya rasimu ya katiba kufanyiwa marekebisho," alisema Masira.
Masira aidha aliongeza kwa kuwarahi wafuasi wa mlengo wa CORD kuwadadisi kiundani wagombezi wa Urais kutoka kwa muungano huo ili kubaini ni yupi ana uwezo wa kupeperusha bendera ya muungano huo.
"Muungano wa CORD ni dhabiti na unaojivunia uungwaji mkono kwenye maeneo mengi nchini, na ni himizo langu kwa wafuasi wa CORD kuhakikisha kwamba wanawadadisi kiundani vinara wa muungano huo ili kubaini ni yupi bora kuwania urais," aliongezea Masira.