Msemaji wa serikali nchini Eric Kiraithe amekanusha madai kuwa polisi wanatumiwa na serikali kuvuruga mikutano ya mrengo wa upinzani wa NASA.
Akizungumza mjini Mombasa, Kiraithe alisema kuwa kauli hizo ni porojo tupu zenye njama ya kuwachanganya wananchi.Kiraithe alisema kuwa polisi hawahusiki kamwe na shutuma hizo bali wanatekeleza majukumu yao kulingana na sheria ya nchi.Aidha, amedai kwamba kuna haja ya viongozi wa NASA kuheshimu serikali na kukoma kueneza uvumi unaoweza leta taharuki na chuki miongoni mwa wananchi, hususan kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi mkuu.Kiraithe aidha amewahimiza maafisa wa polisi nchini kutokubali kutumiwa wala kujihusisha na maswala ya siasa kwani huenda ikasababisha hali ya vurugu ifikapo uchaguzi mkuu.Haya yanajiri baada ya kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kudai kwamba serikali ya Jubilee inatumia maafisa wa polisi kuvuruga mikutano ya upinzani.