Msemaji wa serikali Eric Kiraithe ameonya viongozi dhidi ya kukashifu na kuingiza siasa katika miradi ya serikali.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa, Kiraithe alisema serikali haitaruhusu viongozi wa kisiasa kukashifu miradi ya maendeleo ili kunufaisha malengo yao ya kibinafsi.

Kiraithe alisema ni jukumu la viongozi kuwaeleza wananchi jinsi miradi ya serikali inavyotekelezwa.

Aliwaonywa viongozi dhidi ya kutumia miradi hiyo kuwahadaa wananchi katika misingi ya kisiasa, hatua aliyosema inaathiri maendeleo ya nchi.

“Serikali imejizatiti kikamilifu kutimiza miradi ya maendeleo iliyobuniwa zamani, kwani lengo letu ni kuimarisha maendeleo ya nchi kwa manufaa ya wananchi,” alisema Kiraithe.

Wakati huo huo, amewataka viongozi kubuni miradi itakayowanufaisha wananchi na kuwahimiza Wakenya kujitenga na wanasiasa wanaonunia kuleta mgawanyiko hususan msimu huu wa uchaguzi mkuu.

Akizungumzia swala la walinzi wa wanasiasa, Kiraithe alisema serikali haitaruhusu viongozi hao kuwa na walinzi zaidi kuliko idadi inayoruhusiwa kisheria.

Alisema hatua ya wanasiasa kuwa na walinzi wengi imepelekea wengi wao kuunda vikundi vya kihalifu ili kunufaisha malengo yao ya kibinafsi.