Msemaji wa serikali Eric Kiraithe ametoa onyo kwa wanasiasa wanaowapa vijana dawa za kulevya ili kuzua vurugu katika mikutano ya hadhara.
Akizungumza jijini Mombasa siku ya Alhamisi, Kiraithe alisema serikali itawakabili viongozi hao ambao wanaendeleza biashara hiyo haramu.
“Kuna wanasiasa ambao wanawatumia vijana kwa kuwapa dawa za kulevya ili kuzua vurugu na kuzomea wapinzani wao,” alisema Kiraithe.
Hata hivyo, Kiraithe alidinda kuwataja viongozi hao, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Tutawanasa na kuwafungulia mashtaka viongozi hao,” alisema Kiraithe.
Wakati huo huo, Kiraithe aliyakashifu matamshi ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta, na kusema kuwa miradi inayofanywa kila pembe ya nchi ni kwa manufaa ya wananchi.
“Miradi inayofanywa katika kila kaunti ni kupitia serikali kuu, kwa kuwa serikali kuu ndiyo inayogawa pesa kwa serikali za kaunti,” alisema Kiraithe.
Kiraithe amemtaka Joho kuweka kando tofauti zake za kisiasa dhidi ya mrengo wa Jubilee na kushirikiana na serikali kwa manufaa ya wananchi.
“Joho aweke kando mambo na siasa ili wananchi wa Mombasa wapate maendeleo,” alisema Kiraithe.