Afisa mkuu mtendaji wa maduka ya jumla ya Uchumi Jonathan Ciano, amefungua rasmi zahanati iliyokarabatiwa upya katika makao ya watoto mayatima ya Mama Ngina jijini Kisumu.
Zahanati hiyo, ilikarabatiwa upya, kupitia ufadhili wa maduka hayo ya jumla.
Aidha, Ciano ambaye alikuwa ameandamana na maafisa wengine wa Uchumi, alipeana bidhaa mbali mbali zikiwemo vyakula, dawa na magodoro kwenye makao hayo.
Akiongea na wanahabari wakati wa hafla hiyo mapema Alhamisi, Ciano alisema mradi huo ni mojawapo wa miradi wanaofadhili kila mwaka, kama njia ya kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.
Afisa huyo alisema kuwa katika tamaduni za kiafrika, mtoto ni wa jamii na sharti jamii imlinde.
“Kile tunachofanya ni kuona kuwa watoto wasiojiweza katika jamii, pia wanaishi maisha mazuri. Ukubali ukatae, hawa watoto ndio wataendeleza kizazi kijacho na sharti jamii ijitolee kuwatunza ipasavyo,” akasitiza Ciano.
Amesema kuwa wahudumu wa afya waliohitimu watajiriwa kuhudumu kwenye kituo hicho cha afya, ili kuwa na manufaa makubwa kwa watoto hao mayatima.
Makao ya watoto ya Mama Ngina yanawahudumia watoto wapatao 80, wenye umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka 10.
Kulingana na meneja wa makao hayo Francis OMbogo, makao hayo hufadhiliwa na watu mbali mbali katika jamii, miongoni mwao rais Uhuru Muigai Kenyatta na serikali ya kaunti ya Kisumu.