Hatimaye kituo cha serikali cha ‘Huduma Centre’ kimefunguliwa mjini Nyamira, ambapo kinatarajiwa kuwasaidia wenyeji kwa kuboresha huduma.
Akiongea siku ya Jumatatu wakati wa kufungua rasmi kituo hicho, mkurugenzi wa ‘Huduma’ kutoka serikali kuu Jackline Otwori alisema kuwa ni afueni kwa wananchi ambao wamekuwa wakitembelea afisi mbalimbali kutafuta huduma hizo.
Pia aliongezea kuwa kituo hicho kitakuwa na maafisa kutoka afisi mbalimbali, ambapo sasa wananchi wataweza kupata huduma za serikali kwa urahisi.
“Sasa hiki kituo kitawarahisishia wananchi kazi na mkenya yeyote atapokea huduma mbalimbali anazohitaji bila kupitia changamoto nyingi ilivyokuwa hapo awali,” alisema Otwori.
Kwa upande wake, komishna wa kaunti ya Nyamira Josephine Onunga alisema kuwa ni haki kwa kila mwananchi kuhudumiwa na wafanyikazi wa umma inavyostahili, ambapo aliongezea kuwa mfanyikazi yeyote atakayehusisha na ufisadi atapoteza nafasi ya kazi yake.
“Kuna baadhi ya wafanyikazi wa umma ambao wamezoea maswala ya ufisadi wanapowahudumia Wananchi, afisi yangu itawamulika vilivyo na atakayepatikana atachukuliwa hatua na hata kupoteza kazi,” aliongezea Onunga.