Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa Bahati Nakuru sasa watafaidika kwa huduma bora ya nguvu za umeme kufuatia kuzinduliwa kwa kituo kipya kidogo cha kusambaza nguvu hizo.

Kituo hicho kiligharimu shilingi milioni 387 kwa ushirikiano wa Kenya Power na kaunti ya Nakuru.

Usambazaji wa nguvu za umeme kutoka Kituo hicho kinalenga kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo ya Bahati na viunga vyake.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Alhamisi, naibu gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Ruto alisema kaunti hiyo itakumbatia kikamilifu miradi yote itakayoanzishwa na Kenya Power inayolenga kuboresha maisha ya wakaazi.

“Kwetu sisi, mradi huu unalenga kuleta maendeleo. Kutokana na ongezeko la wawekezaji katika kaunti hii, mradi huu wa kusambaza nguvu za umeme utakuwa rasilmali itakayotumika kikamilifu,” alisema Ruto.

Ruto ameongeza kwamba kaunti ya Nakuru itashirikiana na Kenya Power kuweka taa za barabarani.

Hata hivyo, ameutaka uongozi wa Kenya Power kuwaajiri wafanyikazi zaidi na pia kutumia teknolojia kusoma mita ili kubaini gharama sawia ya utumizi wa nguvu za umeme. Hii ni kuzuia malalamishi ya mara kwa mara kutoka kwa wateja wa kampuni hiyo.

Meneja mkurugenzi na afisa mkuu wa Kenya Power Dkt Ben Chumo alisema kituo hicho kipya kitawahakikishia huduma bora wanaotumia masoko ya Wanyororo na Kabatini pamoja na wakaazi wa Ndundori na viunga vyake.

Chumo pia amehoji kwamba kuna haja ya kuboresha usambazaji wa nguvu za umeme kwa kuwa hilo ni muhimu katika kuhakikisha kuna usalama wa kutosha na maendeleo.

Kenya Power inalenga kuzindua rasmi vituo vingine vidogo 98 vya kusambaza nguvu za umeme kufikia Juni mwaka wa 2016 kupunguza usitishwaji wa mara kwa mara wa nguvu za umeme.