Mbunge wa Njoro Joseph Kiuna amejitenga na sakata ya wauzaji shamba walioripotiwa kulaghai mamillioni ya pesa kutoka kwa wenyeji wa Nakuru katika mpango uliowaahidi kuwamajina yao yangewekwa katika orodha ya watakaopewa makaazi mapya.
Akijitenga na mradi huo, Kiuna akisema kuwa hakuagiza mtu yeyote akusanye pesa kutoka kwa wakimbizi hao wa ndani. Aidha aliwashauri waliolaghaiwa watafute haki kisheria.
Akizungumza na wanahabari mjini Nakuru, mbunge huyo alisema kuwa serikali itawaruhusu waliokuwa wafanyakazi wa Kisima 45 ambao sasa ni maskuota kuwekwa kwenye orodha ya wakimbizi wa ndani ambao watapewa makazi mapya na serikali.
Aliongeza kuwa, kupitia wakili wao, wamefutilia mbali kesi ambayo walikuwa wamewasilisha kortini na kuwarai masaveya kutekeleza jukumu walilopewa la kugawa ardhi na waziri wa Ugatuzi Mwangi Kiunjuri haraka iwezekanavyo ili wakimbizi waweze kupata makazi.
Mwakilishi wa wadi wa Njoro Hezeh Ndung’u aliiomba serikali igeuze mijengo yote iliyo katika ardhi hiyo kuwa mali ya umma kuwasaidia watakaofaidika na mradi huo.