Gavana wa Nyamira ametia saini katika mkataba wa shirika moja lisilo la serikali kutoka nchi ya Ethiopia kwa kusaidia kutengeneza bidhaa zinazotokana na maziwa.
Katika arifa kwa waandishi wa habari siku ya Jumatatu baada ya kutia sahihi ya makubaliano hayo, gavana John Nyagarama, alisema kuwa shirika hilo litajenga kiwanda ambacho kitakuwa kinanunua maziwa kutoka kwa wakulima na kuyatumia kuzalisha bidhaa.
Alisema kuwa wakulima watahitajika kuwasilisha maziwa yao na kulipwa kwa kila kilo au kiwango cha lita watawasilisha.
"Nawaomba wakulima na wafugaji wetu wa Nyamira kujitayarisha kwa kufuga ng'ombe na mbuzi wengi ili mradi huo ukianza wawe na maziwa ya kutosha kuwasilisha kwenye kiwanda hicho," alisema gavana Nyagarama.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Pea Jarni, alimwakikishia gavana Nyagarama kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano na kaunti hiyo ili kuimarisha maisha ya wakaazi pamoja na uchumi kwa jumla.
Huu ni mradi wa tatu kwenye kaunti hiyo mwaka huu, baada ya ule wa umeme wa miale ya jua na mradi wa awali wa kiwanda cha misumari ambacho kilikuwa kianzishwe mwaka huu na wawekezaji wa nchi ya Japan.