Kizaazaa kilishuhudiwa kati ya wakazi wa kaunti ya Nyamira na mawaziri wa kaunti hiyo mnamo siku ya Alhamisi wakati wakazi hao walikuwa wanahitaji kuelezwa bayana kwa nini maendeleo hayajafanywa katika kaunti hiyo.
Mawaziri wa kaunti hiyo waliandaa mkutano na wakazi wa kaunti hiyo, hafla ambayo ilifanyiwa katika shule ya upili ya Sironga, huku mawaziri wakipata mda mgumu kujibu maswali kutoka kwa wakazi kueleza chanzo cha ahadi za maendeleo kutotimizwa hadi sasa tangu mwaka wa 2013.
Wizara zote zilikosolewa kwa kutowajibika kikazi, huku mawaziri wakijaribu kujitetea lakini wakazi hao kuonyesha kutoridhika na majibu ya mawziri hao.
Miongoni mwa wizara ambazo zilikosolewa ni ile ya elimu,afya,barabra na kilimo, huku wakisema wizara hizo hazijafanya chochote na kutaka maendeleo kufanywa kabla ya uchaguzi ujao la sivyo serikali iliyoko kwa sasa isahau uchaguzi ujao.
“Tunahitaji maendeleo kufanywa maana hamna cha kueleza kwa nini hamjafanya maendeleo na pesa ziko ambazo hutumwa na serikali ya kitaifa,” alisema Elkanah Mose, mkazi.