Hafla ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Mugirango-Borabu Okeri Masanya, ilikumbwa na vurugu baada ya vita vya ubabe wa kisiasa kushuhudiwa siku ya Ijumaa.
Haya yalijiri baada ya kundi la vijana kujitwika jukumu la kuchagua atakaye wahutibia waombolezaji waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo.
Shida ilianza Mbunge wa Mugirango Kaskazini Charles Geni alipochukua kipaza sauti ili kuuhutubia umati, ilhali vijana hao walikuwa wamesema kuwa Mbunge wa Borabu Ben Momanyi, ndiye atakayepewa fursa ya kuhutubia wakaazi hao.
Kizaazaa kilizuka huku viongozi kama Charles Nyachae, Mbunge Richard Onyonka na wengine wakitazama kwa mshangao.
Bwana Geni, aliyeghadhabishwa na kisa hicho, aliwakashifu vijana hao kwa kuwaita 'rundo la watu wajinga', kabla ya kuchukua kipaza sauti hicho na kutoroka nacho kutoka kwa jukwaa.
"Mimi ndiye mbunge wa eneo hili na sharti wakaazi waniheshimu. Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi yenu mukikubali kulipwa ili kutupa wakati mgumu. Nyinyi ni rundo la watu wajinga,” Geni alisikika akisema.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya CIC Charles Nyachae, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi ambao walipata fursa ya kuhutubia umati huo, aliwapa wakaazi changamoto kuishi kwa amani na kuepuka kuchochewa wakati wa hafla za mazishi.
"Tulikuja hapa kumuaga mzee lakini nimekasirishwa na vile tulivyojihusisha na siasa za ushindani. Tujiepushe kutumiwa na watu wenye nia ya kujitafutia umaarufu usiofaa. Hii siyo hafla ya uchaguzi na kuanzia leo ni lazima tuheshimu hafla za mazishi,” alisema Nyachae.
Mwenyekiti wa kamati aandalizi Wilfred Nyakundi alikashifu tukio hilo na kuwataka wanasiasa kuwa mfano mwema kwa vijana badala ya kuwapotosha.
"Kama mmoja wa waandalizi, mimi nimekosa maneno ya kuelezea matukio ya leo. Ni aibu kwamba wanasiasa wetu wanaweza kuwatumia vijana vibaya kwa kuwapa rushwa ili kuvuruga mazishi. Tabia kama hii yafaa kukomeshwa,” alisema Masanya.
Marehemu alizikwa masaa ya jioni.