Nusra wawakilishi wadi wa bunge la kaunti ya Nyamira wazabane makonde, baada yao kukosa kuafikia makubaliano ya kujadili ripoti ya kamati ya uwekezaji na uhasibu wa pesa za umma Jumatatu alasiri.
Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo ya PIAC Ezra Mochiemo, baadhi ya wawakilishi wadi hawakutaka ripoti hiyo kujadiliwa wazi mbele ya wanahabari kwa maana baadhi yao wamehongwa ili kuficha ukweli kuhusiana na miradi ghushi iliyoigharimu serikali ya kaunti hiyo mamillioni ya pesa.
"Kuna wawakilishi wadi wengine ambao wamehongwa na maafisa wakuu serikalini ili kutoruhusu ripoti hii ya PIAC kujadiliwa, ila hilo kamwe haliwezi kubaliwa tukiwa hapa kama watetezi wa wanyonge," alisema Mochiemo.
Mochiemo, aliyekuwa akiwahutubia wanahabari nje ya majengo ya bunge la kaunti hiyo aidha alitishia kujiuzulu kutoka kwa kamati ya uwekezaji na uhasibu wa pesa za umma anakohudumu kama mwenyekiti iwapo ripoti hiyo haitajadiliwa mapema jumatano.
"Niko tayari kujiuzulu kutoka kwa wadhifa wa mwenyekiti wa kamati ya PIAC iwapo ripoti hii haitojadiliwa mapema Jumatano ili wakazi wa kaunti hii wafahamu ukweli kuhusiana na jinsi mamillioni ya pesa za miradi zilivyovujwa," aliongezea Mochiemo.
Picha: Mwenyekiti wa kamati hiyo ya PIAC Ezra Mochiemo. Kulizuka kizazaa katika bunge la Nyamira kuhusu ripoti ya utumizi wa fedha. WMaina/Hivisasa.com