Mamlaka ya masuala ya baharini KMA imepinga madai ya ufisadi dhidi yake kama ilivyodaiwa na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu mapema wiki hii.
Mapema Jumatatu wiki hii, mashirika mbalimbali yalifanya maandamano nje ya ofisi za mamlaka hiyo yakishinikiza kufungwa kwa ofisi hizo kutokana na madai ya ufisadi.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano, mamlaka hiyo ilipinga madai ya kutoa zabuni kwa njia za upendeleo kama ilivyodaiwa.
“Tunashauri ikiwa kuna mtu mwenye lalama zozote kuwasilisha kupitia kwenye bodi maalum inayohusika badala ya kuandaa maandamano,” taarifa hiyo ilieleza.
Kuhusu swala la kuajiri wafanyikazi, mamlaka hiyo ilijitetea ikisema kuwa zoezi hilo huendeshwa kwa uwazi kulingana na katiba na pia sheria za mamlaka hiyo.
Kati ya mashirika yaliyoshiriki katika maandamano hayo ya Jumatatu ni Mombasa Civil Society Forum lililodai kuwepo kwa visa vya ufisadi, upendeleo na matumizi mabaya ya mali ya umma.