Baraza la kitaifa la mitihani nchini (KNEC) limeahidi kuvikabili visa vya udanganyifu wakati wa mitihani na kuwasilisha matokeo halali ya mitihani mwaka huu.
Akizungumza kwenye kongamano la walimu wakuu lililoingia siku yake ya pili mjini Mombasa siku ya Jumanne, mwenyekiti wa KNEC Prof George Magoha, alisema baraza hilo litafanya kila liwezalo kutokomeza uovu huo ili kumpa kila mtoto fursa ya kufaulu maishani.
“Hatutawaruhusu wanafunzi wengine kutumia njia za mkato kupita ilhali wenzao wanatumia akili na bidii zao. Safari hii tumeweka mikakati dhabiti itakayohakikisha kuwa mianya yote inayotumika kuiba mtihani huo imezibwa,” alisema Magoha.
Aidha, Magoha amewataka walimu wakuu kote nchini pamoja na wadau wengine wa sekta ya elimu kuunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na wizi wa mitihani.
Akiongea katika hafla hiyo waziri wa elimu Dr Fred Matiang’i alikariri kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa matokeo ya mtihani wa mwaka huu yatakuwa halali na ya kuaminika.
Naye mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu elimu, utoaji mafunzo na utafiti Sabina Chege, amewataka walimu wakuu kushisirikiana na idara zingine za elimu ili kuzuia wizi wowote wa elimu kutokea.