Baraza la mitihani nchini KNEC limeshinikizwa kuangazia upya sheria za mitihani nchini kuzuia visa vya wanafunzi kutoroka shuleni mara tu baada ya kusajiliwa kwa mitihani ya kitaifa.
Shinikizo hizo zilitokana na kushuhudiwa kwa idadi kubwa ya wanafunzi kaunti ya Mombasa, Kilifi na Taita Taveta ambao hutoweka shuleni baada ya kusajiliwa, hali ambayo inachangia matokeo duni katika mitihani ya kitaifa.
Mwito huo ulitolewa na mwenyekiti wa walimu wakuu wa shule za upili katika muungano wa kaunti hizo tatu, Boniface Karisa katika kongamano la elimu mjini Mombasa siku ya Ijumaa aliposema kwamba tabia hiyo huathiri matokeo ya mitihani ya kitaifa.
“Tunataka KNEC kubuni sheria mpya zitakazoangazia maswala ya mitihani pamoja na kuzuia wanafunzi kutoroka shuleni baada ya kusajiliwa katika mitihani ya kitaifa kwani wengi wao hukosa kufanya mitihani hiyo,” alisema Karisa.
Karisa ameonya kuwa iwapo hakutakuwa na sheria mwafaka za kuzuia visa hivyo, wanafunzi wa jamii nyingi mashinani watasalia nyuma kielimu.
“Iwapo hakutakuwa na sheria hiyo basi wanafunzi wengi wataishikia kujiunga na makundi ya kihalifu na wengine watatumia hata mihadarati kwa sababu wamekosa msingi bora wa elimu pamoja na kutokuwa na vyeti vya elimu vitakavyowasaidia katika kutafuta hata ajira,” aliongeza Karisa.
Muungano huo umependekeza kuidhinishwa sheria kali za kuwazuia wanafunzi kusalia shuleni na kufanya mitihani yao ya kitaifa ili kuwawezesha kutimiza ndto zao katika siku za usoni.