Baraza la mitihani nchini Knec na Wizara ya Elimu nchini zimetakiwa kujadiliana kwa kina na kurejelea usahihishaji wa mitihani ya kitaifa ya wanafunzi waliyohusishwa na visa vya udanganyifu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu wa Chama cha Knut tawi la Mombasa Dan Aloo amesema kuwa itakuwa sio vyema kwa wanafunzi hao zaidi ya 5,500 kukosa matokeo yao ilhali serikali ina mbinu mbadala ya kurekebisha matokeo hayo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Aloo alisema kuwa iwapo vijana hao waliomaliza masomo yao watajiunga na uhalifu, basi serikali na baraza la mitihani nchini ndizo zitalaumiwa kuwa kukosa kuzingatia mapendekezo ya baadhi ya wadau wa sekta ya elimu nchini.

Aloo alisema kuwa serikali inafaa kulizingatia swala hilo ili kuwasaidia vijana hao kupata matokeo yao na kufanikisha ndoto zao.

Alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha vijana kujihusisha na maswala muhimu ya kuendeleza taifa hili kiuchumi.

“Tunamtaka Waziri wa Elimu nchini Dkt Fred Matiangi na maafisa wakuu wa baraza la mitihani nchini Knec kuzingatia mapendekezo yetu kama wadau wa sekta ya elimu na kuwasaidia vijana hawa kupata matokeo yao ya mitihani ya kitaifa. Sio jambo kubwa kuagiza walimu waliosaihisha mitihani hiyo kurejelea zoezi hilo ili wanafunzi wasaidike na kutimiza lengo lao katika siku za usoni,” alisema Aloo.

Wadau hao wa sekta ya elimu nchini wameahidi kuishinikiza serikali kuhakikisha kuwa swala hilo linangaziwa ili kuwasaidia vijana hao kuweza kujikimu kimaisha.