Katibu wa Chama cha KNUT tawi la Mombasa Dan Aloo, ameyakosoa maagizo ya Waziri wa Elimu nchini Dkt Fred Matiang’i.
Aloo amekosoa hatua ya Matiang’i ya kupiga marufuku likizo fupi katika muhula wa tatu, pamoja na hafla za maombi kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani yao ya kitaifa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Aloo alisema maamuzi kuhusu masuala yanayogusia sekta ya elimu moja kwa moja yanastahili kuwahirikisha wadau wote wa sekta hiyo nchini.
Aloo alisema hatua ya Waziri Matiang’i kamwe haitasaidia kuzitatua changamoto katika sekta ya elimu nchini, hususan visa vya wizi wa mitihani.
Katibu huyo alisema kwamba matatizo yanayolikumba Baraza la Mitihani Nchini KNEC, sharti yaangaziwe ndipo visa vya wizi wa mitihani viweze kudhibitiwa.
Wakati huo huo, Aloo amemkosoa Matiang’i kwa kutolishughulikia suala la malipo ya walimu ambao walisimamia mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE ya mwaka jana kwa wakati ufaao.
“Mwanzo tunamtaka Matiang’i kuangazia malipo ya walimu waliosimamia mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE ya mwaka jana, kabla ya kutoa maagizo yake anayodai yatasaidia kuzuia wizi wa mitihani,” alisema Aloo.